Ni muhimu kuzingatia utunzaji wa vifaranga

Ni muhimu kuzingatia utunzaji wa vifaranga

Vifaranga waliyotunzwa vizuri
Vifaranga wanapotunzwa vizuri kama hawa hukua vizuri na kuwa kuku wenye afya

Kwa karne na miaka mingi, ufugaji wa kuku imekuwa ni kazi muhimu na inayokubalika katika jamii nyingi. Ni kazi isiyohitaji gharama kubwa sana, ambayo imekuwa na mafanikio kwa kiasi kikubwa kwa wanaiofanya kibiashara.

Tatizo ambalo limekuwa sugu na kusababisha hasara kwa wafugaji walio wengi, ni kutofahamu namna bora ya kuwatunza vifaranga kuanzia siku ya kwanza wanapoanguliwa hadi kuwa kuku wakubwa. Hali hii imekuwa ikiwasababishia wafugaji hasara na kuwakatisha tamaa.

Hii inatokana na wafugaji kuzingatia kuwa na banda na chakula tu, bila kuzingatia aina nyingine ya matunzo muhimu yanayohitajika kwa ajili ya kuwafanya vifaranga waishi na kukua wakiwa na afya.

Haya ni baadhi ya mambo muhimu kuanzia siku ya kwanza ili vifaranga wako wasipate madhara na hatimaye kufa:

• Mara baada ya kuanguliwa, vifaranga wawekwe sehemu yenye joto kwa wastani unaohitajika.Kuku wenye afya 1
• Hakikisha sehemu ya banda ulipowaweka vifaranga ni kavu, na isiyokuwa na vimelea.
• Hakikisha vifaranga wote wanapata chanjo ya mahepe (mareks) siku ya kwanza.
• Siku ya saba, vifaranga wachanjwe dhidi ya ugonjwa wa kideri.
• Inapofika siku ya 14, vifaranga wachanjwe dhidi ya ugonjwa wa gumboro.
• Rudia chanjo ya kideri katika siku ya ishirini na moja.
• Siku ya ishirini na nane, rudia tena chanjo ya gumboro
• Baada ya wiki nane, hakikisha kuwa vifaranga wako wanapata chanjo ya ndui.

Kwa kuzingatia mtiririko huo, utakuwa na uhakika kuwa kuku wako ni salama. Watakuwa bila tatizo, jambo ambalo litakupa uhakika wa kuwa na mazao bora, na hatimaye kupata faida.
Pamoja na hayo, hakikisha kuwa unazingatia lishe bora. Hii itasaidia kuwapa kuku afya njema na kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa.

**Kamwe usiwape kuku vyakula vilivyooza. Hii inaweza kusababisha madhara makubwa kwa kuku na kusababishia hasara.

Zalisha Matango uboreshe kipato kwa muda mfupi

Matango (cucumber) ni zao muhimu katika mazao ya mboga na matunda nchini Tanzania na hata nje ya Tanzania.

Cucumber
Ni vizuri kuwekea matango fito kwani matunda yake yakilala ardhini huoza.
Hili ni zao la biashara, pia chakula. Zao hili hustawi na kulimwa kwa wingi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Pwani.


Matumizi:  Matango hutumika kama tunda, ijapokuwa ni aina ya mboga na huongeza vitamin A, C na maji mwilini. Pia, tango linaweza kutumiwa kama saladi wakati wa mlo.


Hali ya hewa: Matango hustawi kwenye hali ya joto, hali kadhali kwenye sehemu yenye joto kidogo pia hustawi. Matango yanahitaji joto wastani wa nyuzi joto 20°C – 25°C. Zao hili pia huhitaji maji kwa wingi, ingawa unyevu ukizidi husababisha magonjwa kwenye majani na maua.


Udongo:  Kwa ustawi mzuri wa matango, udongo unatakiwa kuwa na rutuba ya kutosha, na chachu ya kuanzia 5.5 hadi 6.7, mwinuko unaotakiwa ni kuanzia mita 1000-1200 kutoka usawa wa bahari.

Tofauti na ilivyo mazao mengine, matango hayahitaji mwanga mkali sana kwa kuwa husababisha maua dume kuzaliwa, hivyo kuathiri uzalishaji wa idadi ya matunda ya matango. Mwanga kidogo husababisha maua jike kuchanua kwa wingi kuongeza kiwango cha mazao. Mwanga unapokuwa mwingi, inabidi kutumia neti au aina nyingine ya vizuizi ili kupunguza mwanga, ambapo pia itasaidia kulinda mmea dhidi ya upepo mkali ambao unaweza kuharibu maua na matunda, au mmea kwa ujumla.


Kupanda: Mara nyingi matango hupandwa moja kwa moja shambani. Wakulima wengine hupanda kwenye vitalu au makopo na baadae kuhamishia miche inapofikia sentimita 8-12. Endapo mbegu zimepandwa shambani moja kwa moja, inatakiwa ipunguzwe na kubakia mche mmoja tu kwenye kila shimo.

Nafasi: Nafasi kati ya mche na mche ni sentimita 60-70, na nafasi kati mstari na mstari ni sentimita 70-90. Mimea inatakiwa iwekewe miti ili iweze kuzaa matunda mengi na kuepuka kukaa chini ambapo matunda yanaweza kuoza au kuharibiwa na wadudu.

Mbolea:  Mbolea ni muhimu sana, kabla ya kupanda au kuhamisha miche. Mbolea inayoweza kutumika ni samadi au ya viwandani isiyokuwa na madhara kwa mazingira na afya ya binadamu. Baada ya kupanda, tumia mbolea ya maji maji kila baada ya siku 14-21, mpaka mmea uweke matunda.


Palizi: Palizi ni muhimu , ili kuepuka magonjwa na kunyang’anyana chakula kati ya zao na magugu.


Wadudu waharibifu: Wadudu waharibifu wa matango ni pamoja na Vidukari, inzi weupe, na minyoo ya mizizi.


Magonjwa: Magonjwa yaliyozoeleka kushambulia matango ni pamoja na Ukungu, fusari, na magonjwa ya virusi.


Kuvuna:  Matango yanaweza kuwa tayari kuvunwa kuanzia siku 50-60 na matunda yanatakiwa yawe na urefu wa sentimita 15 mpaka 20. Makadirio ya mavuno ni tani 6 kwa ekari moja.

Ufugaji wa Samaki Kwenye Bwawa


Bwawa la maji 1
Wakulima wanaweza kuongeza kipato kutokana na ufugaji wa samaki katika maeneo yao
Ufugaji wa samaki kama ilivyo shughuli nyingine yoyote ya kiuchumi inahitaji usimamizi mzuri ili uweze kuwa na faida. Mbali na hilo, mfugaji wa samaki anatakiwa kuzingatia vigezo vingi kabla ya kuanza ufugaji. Moja ya vigezo hivyo ni soko. Si jambo la busara kuanza shughuli yoyote kabla haujafanya uchunguzi na kujua kama kuna mahitaji ya bidhaa unayokusudia kuzalisha. Wafugaji wengi wameanzisha ufugaji wa samaki lakini wakaishia kupata hasara kutokana na ukosefu wa soko. Na wengine wameanguka kutokana na utunzaji mbovu wa mabwawa ya samaki.

Maji
 Upatikanaji wa maji na ubora wake ni kigezo muhimu katika ufugaji wa samaki. Mtiririko wa maji ni njia rahisi kwa mfugaji. Maji machafu hayatakiwi kwa ufugaji wa samaki. Wafugaji ni lazima wasaidiwe na maafisa kilimo katika eneo lao kama maji yanayopatika yana ubora kwa ajili ya ufugaji wa samaki. Kwa wakazi wa Dar es
Salaam, inawezekana pia kufuga samaki kwenye bwawa, endapo maji yana chumvi ya wastani, na kwa kiwango kinachoshauriwa kitaalamu, basi samaki wanaweza kustahimili, na kukua vizuri.

Bwawa

Bwawa la samaki linahitaji nafasi kubwa ya ardhi, yenye mwinuko pamoja na eneo la samaki kukimbilia. Hii ni njia rahisi ya ufugaji endapo ardhi na maji havina gharama kubwa. Eneo kubwa zaidi linaruhusu uzalishaji usiohitaji nguvu ya ziada na wenye tija.

Utengenezaji wa bwawa la samaki kwa maeneo yenye udongo wa kichanga kama Dar es Salaam, mfugaji atalazimika kuchimba na kuweka karatasi ya nailoni. Hii, itasaidia kuzuia upotevu wa maji pamoja na kuzuia bwawa kuporomoka.

Ni vyema upande mmoja wa bwawa ukawa na kina kirefu kuliko mwingine. Upande mmoja unaweza kuwa na kina cha mita moja na nusu, na mwingine mita moja. Hii itamsaidia mfugaji kuweza kulihudumia bwawa vizuri, hata kama ni kuingia na kufanya usafi.

Utunzaji wa bwawa

Samaki 1Inashauriwa kufanyia bwawa usafi mara kwa mara, hasa kwa kuondoa majani ili kuepusha wadudu kufanya makazi na hatimaye wakawadhuru samaki. Pia ukiacha mimea bwawani itatumia virutubisho kwa kiasi kikubwa na kuondoa hewa ya oxijeni.
Hivyo, kila unapoona uchafu, safisha mara moja.

Ulishaji

Wafugaji walio wengi, wamekuwa hawazingatii kanuni za ulishaji wa samaki. Kwa kawaida inatakiwa kuwalisha samaki mara mbili hadi mara tatu kwa siku.

Aina ya chakula

Samaki wanaweza kulishwa kwa kutumia pumba ya mahindi, mashudu ya pamba na alizeti, soya, mabaki ya dagaa. Haishauriwi kulisha chakula kilichoko kwenye mfumo wa vumbi, bali kiwe mabonge madogo madogo, kwa wastani wa tambi.

Magonjwa

Kwa kawaida samaki hawana magonjwa mengi sana yanayowashambulia, ila kuna baadhi ya yaliyozoeleka kama vile magonjwa ya ukungu (fangasi), magonjwa yatokanayo na virusi, pamoja na minyoo.

Samaki wanaposhambuliwa na fangasi, huonekana kwa macho kwa kuwa huwa na madoa madoa. Samaki aina ya kambale hushambuliwa zaidi kuliko perege.

Pia unaweza kutambua kuwa samaki ni mgonjwa kwa kuwa huzubaa sehemu moja kwa muda mrefu. Magonjwa kwa samaki pia yanaweza kutokana na mrundikano kwenye bwawa. Hivyo, ni muhimu kuwapunguza kila wanapoongezeka.

Tiba

Tiba iliyozoeleka kwa samaki ni kwa kuweka chumvi kwenye maji, kasha kuwatumbukiza samaki unaowaona kuwa ni wagonjwa, kisha kuwatoa na
kuwarudisha bwawani.

Upatikanaji

Unaweza kupata vifaranga wa samaki kutoka katika kituo cha kuzalisha na kufuga samaki Kingolwira Morogoro. Bei ya kifaranga cha Perege ni shilingi 50, na Kambale ni shilingi 150.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na Bwana Kalinga kwa simu namba 0757891 761, 0787 596 798