Kilimo cha Parachichi: Pandikiza parachichi upate mavuno zaidi

Msukumo wa uhitaji mkubwa wa parachichi kwa wingi na zenye ubora unawasukuma wakulima kutumia teknolojia mpya.

Upandikizaji hujumuisha aina mbili za mimea. Unachukua mmea mmoja ambao unadhani hauna tija nzuri, na sehemu ya mmea mwingine ambao una ubora zaidi na kupandikiza kwa kukata na kufunga pamoja ili kupata mbegu bora zaidi. Utaratibu wa kupandikiza hivi sasa umekuwa silaha ya wakulima kuwakomboa dhidi ya wadudu pamoja na magonjwa, na hili kwa sasa halifanyiki tena maabara kama ilivyokuwa awali na hii inadhibitishwa na yale tuliyojionea Njombe tulipotembelea wakulima.

Kwenye shamba la bwana Bosco Kidenya, ana kitalu chenye zaidi ya miche 1200 ya miparachichi, baadhi ikiwa tayari imeshapandikizwa na mingine ikiwa inasubiri kufikia wakati wa kupandikiza.  Huyu ni mmoja kati ya wakulima walio wengi wanaofanya kazi kwa karibu na CARITAS Njombe, kuboresha uzalishaji wa parachichi, pamoja na kuboresha kipato cha wakulima ambao wanazalisha matunda na mboga mboga.

Mbinu wanayotumia

Wakulima hukusanya kokwa za parachichi kutoka maeneo ya sokoni; wanachofanya ni kuhakikisha tu kuwa mbegu hiyo ni safi, haijaathiriwa na magonjwa na itaota. Baada ya hapo huchagua zile zenye muundo mzuri na kuzipanda kwenye boksi au kwenye sehemu ya kitalu. Baada ya kuota huziotesha kwenye makopo, au kwenye viriba kisha kuendelea kumwagilia maji mpaka zinapokuwa na umbo usawa wa penseli. Upandikizaji ni lazima ufanyike wakati mmea umefikisha unene wa penseli. Kupandikiza kwa kutumia chipukizi lililolingana na mche unaopandikizia ni njia yenye mafanikio zaidi.

Upandikizaji ni lazima ufanyike wakati ambao mizizi bado ni laini. Pandikizi litakalotumika wakati wa kupandikiza ni lazima lisiwe katika hatua ya ukuaji kwa wakati huo, na ni lazima umbo liwiane na mti linapopandikizwa kuzuia maji yasipotee na kusababisha pandikizi kukauka.

Mapandikizi ni lazima yatokane na aina ya parachichi ambazo zimeboreshwa kama vile hass, fuerte  au puebla. Kwa wale wakulima ambao mmea utatoa majani mapya. wana mkataba na Africado, watahitajikupata mapandikizi kutoka kwenye miti ya hass. Hii ina maanisha kuwa mkulima anayetaka kuanzisha kitalu kwa ajili ya kupandikiza ni lazima apande walau miti 5 ya parachichi aina ya hass ili kupata mapandikizi.

Njia ya kupandikiza ina ufanisi zaidi na ni rahisi kuliko kupanda miche upya, kwa kupandikiza inagharimu chini ya asilimia 75, kuliko kupanda miche upya na kuweza kupata aina ambayo inastahimili magonjwa. Wakulima pia wamekuwa na rikodi nzuri ya ongezeko la mavuno kutokana na mimea waliyopandikiza, pamoja na upungufu wa matumizi ya madawa.

Wakulima ambao wanafanya kazi zao chini ya CARITAS Njombe sasa wanaona faida kubwa inayotokana na kupandikiza, wameamua kuwekeza kwenye utaalamu huu na kuwa na miche mingi kwenye vitalu vyao. Hii ni mbinu ya kilimo ambayo ina faida kubwa kwa mkulima, huku akiwa amewekeza kwa kiasi kidogo sana katika kukabiliana na wadudu na magonjwa na kuepuka kuwa na mazao yenye ubora wa chini.

Namna ya kupanda

 Nafasi halisi inayohitajika na mmea wa parachichi ili ukae vizuri ni nafasi ya 9m x 9m. Chimba shimo katika vipimo vya 60sm x 60sm kwa 60sm kwenda chini kisha tenga udongo wa juu na wa chini. Changanya udongo wa juu na mbolea ndoo moja iliyooza vizuri, pamoja na kiganja kilichojaa cha mbolea ya minjingu.

 Ondoa mche wako kwenye kiriba ulipopandwa. Hii itakuwa rahisi zaidi endapo ulikuwa umenyweshea muda kidogo uliopita. Panda kwa kutumia udongo wa juu uliochanganya na mbolea na uweke mpaka kujaza shimo.

 Mwagilia maji mara baada ya kupanda. Funika mmea mchanga kwa kutumia majani ya migomba au aina nyingine ya majani yanayofanana na hayo, mpaka kufikia kipindi ambacho mmea utatoa majani mapya.

Kilimo: Utunzaji wa udongo kwa ajili ya kilimo hai

Uelewa wa maisha ya mimea husaidia kwa kiasi kikubwa kwa hatua ya kuchukua kuilisha mimea hiyo.

Utunzaji wa udongo unategemeana kwa kiasi kikubwa na mazingira ya kibiolojia. Kazi kubwa ya baadhi ya viumbe hai waliomo kwenye udongo, ni kumeng’enya mabaki ya mimea na viumbe hai wengine. Mtiririko huu hufanya uwepo wa nguvu, virutubisho, na hewa ya kaboni, ambavyo kwa pamoja hutengeneza rutuba kwenye udongo.

Utunzaji wa rutuba ya udongo unaongozwa na filosofia hii ‘Lisha udongo ili nao ulishe mimea.’ Udongo wenye rutuba utazalisha mimea yenye afya inayoweza kukabiliana na magonjwa. Uzalishaji wa mazao kwa njia za asili uhakikisha kunakuwepo uzalishaji wa kutosha bila ya kutumia pembejeo za ziada isipokuwa matandazo, mboji na bila kutifua udongo mara kwa mara. Ongezeko la malighafi za asili husaidia kuimarisha udongo na kufanya kuwepo kwa virutubisho vya kutosha.

Athari kwa afya ya mimea

Kwa bahati mbaya, aina ya kilimo cha kisasa na kinachotumia kemikali hufanywa tofauti na ilivyo kwa kilimo hai. Katika aina hii ya kilimo; udongo hulimwa mara kwa mara jambo linalosababisha uharibifu wa muundo wa udongo, uwiano wa virutubisho, ambapo virutubisho huongezwa kwa kutumia mbolea za viwandani na matandazo hayazingatiwi. Muundo wa udongo unapobadilika, rutuba nayo hupungua, uwezo wa udongo kwenye udongo pia hupungua.

Kiwango cha udongo mzuri pia hupungua kwa kuwa hakuna tena viumbe hai wanaotengeneza udongo ila unapungua kila msimu wa mavuno. Kwa asili mzunguko huu huwa na matokeo yanayoishia kwenye afya ya mimea, na hapa wadudu huchukua nafasi inayowawezesha kufikia malengo yao.

Ziba pengo

Wakulima wanatakiwa kuhakikisha kuwa kuna virutubisho vya kutosha shambani mwao kila wakati. Ikiwa kuna mwanya pale ambapo baadhi ya pembejeo zinakosekana, kununua virutubisho kwa ajili ya udongo vilivyomo kwenye mfumo wa mbolea za asili inaruhusiwa. Hata hivyo, weka utaratibu wa kuwa na virutubisho kutoka shambani mwako muda wote.

Endapo tukitegemea kulisha udongo kutokana na mbolea za viwandani na kutumia virutubisho vya asili, bado tutakuwa tunafanya sawa na yanayofanyika katika kilimo cha kisasa. Tutakuwa hatujauongezea udongo uwezo wa kujitengeneza na kuongezeka, jambo ambalo ndio msingi muhimu wa kilimo hai.

Vyanzo vya virutubisho

Mimea inayofunika udongo – Mimea inayotambaa huongeza na kushika virutubisho kwenye udongo,kuongeza malighafi zinazooza kwenye udongo, kuzuia madini ya naitraiti kuzama kwenye udongo, virutubisho kutiririshwa, na mmomonyoko wa udongo. Jambo la muhimu hapa ni kuwa udongo umefunikwa ili kuzuia uharibifu. Mimea jamii ya mikunde inapendekezwa zaidi kwa kuwa
husaidia kuongeza nitrojeni kwenye udongo inayopatikana hewani.

Inashauriwa pia kuchanganya mimea jamii ya mikunde na nyasi kwa kuwa nyasi hutumia nitrojeni nyingi sana kutoka kwenye udongo, hivyo itasaidia kutokuharibika kwa mtiririko mzima wa uwekaji wa nitrojeni kwenye udongo.

Mboji - Mboji hasa inayotengenezwa kwa kutumia kinyesi cha wanyama, inaweza kuwa chanzo kizuri cha viumbe wadogo kwenye udongo na virutubisho vyenye gharama ndogo. Unapotumia mboji, changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa imeoza vizuri na namna ya kuitumia kwa usahihi. Endapo mchanganyiko uliotumika kutengeneza mboji hiyo yalikuwa na ubora wa chini, basi mboji hiyo nayo itakuwa na ubora mdogo sana. Itakuwa vizuri kama wakulima hawataacha mboji ikapigwa na jua au mvua, kwa kuwa hali hii inaweza kusababisha kupotea kwa virutubisho kwenye mboji. Kinyesi cha mifugo huboresha mboji zaidi.

Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa kiasi cha 15% ya virutubisho vinavyopatikana kwenye mboji hutumika shambani kwa mwaka wa kwanza. Hivyo, matumizi ya mara kwa mara ya mboji yanapendekezwa ili kuweza kuongeza nitrojeni na malighafi zinazo oza kwenye udongo.

Samadi - Samadi inayotokana na wanyama waliokomaa inaweza kuwa na uwiano mzuri wa virutubisho vya nitrojeni na aina nyingine kwa kiasi kidogo. Tatizo moja la samadi ni upatikanaji pamoja na kutokuwa na ubora unaofanana wakati wote. Kiasi kikubwa cha samadi inayotumika kwenye shamba la mboga, huozeshwa kabla ya kutumika, jambo linalosaidia kupunguza madhara kwenye vyakula.

Malengo kwa ajili ya udongo na mazao
•  Kuongeza malighafi zinazo oza kwenye udongo
• Kuboresha muundo wa udongo
• Kuwezesha upatikanaji wa nitrojeni
• Kuongeza uwezo wa uhifadhi wa rutuba
• Kujenga uwepo wa uhai wa viumbe hai kwenye udongo
• Kufifisha magonjwa ya mazao
• Kujenga mazingira ya udongo wenye uwiano

Kilimo Alizeti: Alizeti ni chanzo cha malisho ya mifugo

Alizeti haitoi mailisho pekee, pia inatoa mafuta bora kwa afya ya binadamu na pia malighafi inayotumiwa na nyuki kutengeneza asali.
Unapotengeneza chakula cha mifugo peke yako, si tu kupunguza gharama, lakini pia inakupa uhakika wa kuwa na chakula bora. Pia Wafugaji wa nyuki wanaopanda alizeti wanapata faida ya ziada kwa kupata asali iliyo bora kwa sababu nyuki hukusanya poleni kutoka kwenye alizeti wanapofanya ushavushaji.

Chanzo kizuri cha protini

Chakula cha mifugo kinachotengenezwa kutokana na alizeti ni chanzo kizuri cha protini kwa ajili ya mifugo, hasa ng’ombe wa maziwa, kuku, nguruwe na hata sungura. Malisho haya yana kiasi kikubwa cha protini, nyuzi nyuzi na kiasi kikubwa cha mafuta. Malisho haya yana protini kiasi cha asilimia 29-30, kiasi cha nyuzi nyuzi asilimia 27-31.

Moja ya tabia nzuri ya alizeti ni kwamba haina vitu vinavyoathiri virutubisho kwa mifugo, hata hivyo, ina kiasi kikubwa cha nyuzi nyuzi na mashudu yake kuwa magumu kiasi, jambo ambalo husababisha ugumu kidogo kwenye kusagwa tumboni. Mbali na virutubisho vya aina nyingine, alizeti ni chanzo kizuri cha kalishamu, fosiforasi na vitamini B.

Ubora wa alizeti inayotumika kwa ajili ya malisho ya mifugo inategemeana na namna ambayo imetayarishwa. Kwa mfano, alizeti inayosagwa bila kuondoa maganda ya nje, ina kiasi kikubwa cha nyuzi nyuzi (kati ya asilimia 27-30, lakini inakuwa na kiasi kidogo cha protini asilimia 23). Alizeti ambayo imetayarishwa kwa ubora wa hali ya juu huwa maganda yameondolewa na inakuwa na kiasi kikubwa cha protini, kiasi cha asilimia 40.

Mkulima anapaswa kufahamu kuwa alizeti bado inakuwa na virutubisho hata kama haitatayarishwa kwa ustadi. Mfugaji anaweza kutumia soya na karanga badala ya alizeti, lakini ni lazima apeleke alizeti kupima kuhakikisha kuwa ina nyuzinyuzi na virutubisho kwa kiwango cha nyuzinyuzi na protini kinachokubalika.

Inapendekezwa kutumia alizeti

Kulingana na utafiti ambao umefanyika nchini Tanzania, alizeti iliyochanganywa na pumba ya mahindi kwa kiasi cha asilimia 30, kisha kulishwa ng’ombe aina ya Zebu ina uwezo wa kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 6.6 kwa siku mpaka lita 8.1 kwa siku. Nchini Zimbabwe, mashudu ya alizetu huchanganywa na mahindi pamoja na  mabua ya mahindi ambayo yamewekwa urea kwa kiwango cha wastani wa kilo 4.4 kwa siku, na kulishwa ng’ombe aina ya Jersey pamoja na ng’ombe chotara ambao hulishwa katika machungo ya wazi, Ng’ombe hawa huongeza kiasi cha maziwa kwa wastani wa kilo 5.8 mpaka kilo 6 kwa siku.

Aina ya alizeti

Kuna aina mbili za alizeti, alizeti fupi na alizeti ndefu. Aina ndefu hurefuka mpaka kufikia kiasi cha urefu wa mita 1.5-2.4. Uzalishaji wake ni hafifu ukilinganisha na mbegu za kisasa. Aina hii mara nyingi huwa ile inayojulikana kama Hungary nyeupe na Fedha. Alizeti fupi ni inayotokana na mbegu za kisasa ambayo huwa na urefu wa mita 1.2, aina hii huwa na mavuno mazuri zaidi ukilinganisha na aina ndefu.

Kutengeneza chakula cha mifugo

Kilo tatu na nusu za alizeti inapokamuliwa hutoa mafuta lita moja na mashudu kilo mbili na nusu.

Resheni kwa ng’ombe wa maziwa

•Changanya kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi ili kutengeneza chakula cha ng’ombe.
•Mlishe ng’ombe anaezalisha maziwa kwa wingi kiasi cha kilo 4 ya mchanganyiko huo na kilo 2 kwa ng’ombe anaezalisha kiasi kidogo cha maziwa.
•Mbali na kulisha mchanganyiko huo, ng’ombe wa maziwa ni lazima apewe kiasi kingine cha chakula cha kawaida cha kila siku kama vile matete, hay, au aina nyingine yoyote ya malisho bora kwa kiasi cha kutosha.

Resheni kwa ajili ya kuku

Chakula cha kuanzia: Changanya kilo 22 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi Chakula cha kukuzia: Changanya kilo 20 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi au chenga.
Chakula kwa ajili ya kuku wanaotaga: Changanya kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za chenga za mahindi

ZINGATIA: Unapotengeneza chakula kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa mashudu hayazidi asilimia 20 ya resheni ya kulishia. Kwa ajili ya kulishia kuku, alizeti isizidi asilimia 7 ya jumla ya resheni.

Namna ya kuzalisha alizeti

Hali ya hewa: Alizeti hustawi vizuri zaidi kwenye udongo tifutifu, wenye rutuba ya kutosha. Zao hili lina mizizi inayoenda chini kwa kiwango cha kikubwa hivyo kuiwezesha kustawi hata katika sehemu yenye kiwango kidogo cha mvua. Kiasi cha wastani wa milimita 500-750 za mvua zinatosha kabisa kwa uzalishaji wa alizeti. Inaweza kulimwa kutoka usawa wabahari mpaka kufikia mwinuko wa mita 2600 kutoka usawa wa bahari.

Maandalizi ya shamba

Ni lazima kuhakikisha kuwa shamba limelimwa vizuri, ili kuweza kupata sehemu nzuri ya kusia mbegu.
Nafasi: Mbegu zinaweza kupandwa kwa nafasi ya sentimita 75 kwa 30 kwa kiasi cha kilo 2 kwa ekari moja (sawa na kilo 5 kwa hekari). Panda mbegu 3 kwa kila shimo, kisha acha mmea mmoja kwa kila shimo mimea inapofikia urefu wa sentimita 10-20.

Matumizi ya Mbolea

Alizeti hufanya vizuri kwenye udongo wenye rutuba. Matumizi ya mbolea inayotokana na miamba aina ya fosifeti inafaa zaidi kwa kuwa alizeti inahitaji fosifeti kwa kiasi kikubwa. Matumizi ya mbolea mboji iliyoandaliwa vizuri itaongeza virutubisho vya ziada kwenye udongo.
Alizeti hukua vizuri katika sehemu isiyokuwa na magugu. Palilia alizeti inapokuwa na urefu wa mita 0.7 (Kiasi cha wiki 4).

Ndege waharibifu

Ndege wanaweza kuharibu kiasi cha asilimia 50 ya alizeti endapo hawatafukuzwa. Ili kuzuia uharibifu huo, mkulima anaweza kuchukua hatua zifuatazo;
•Vunja shina la alizeti kufikia usawa wa magoti kabla ya alizeti kukauka. Unaweza pia kuvunja katika urefu wowote lakini alizeti iangalie chini ili kuzui ndege kudonoa.
• Ondoa alizeti shambani baada ya kukauka na kuihifadhi.
• Ubanguaji unaweza kufanyikia nyumbani kwa kutumia fimbo
• Alizeti ni lazima ikaushwe mpaka kufikia kiwango cha unyevu wa asilimia 10 kabla ya kuhifadhiwa

Ufugaji Ng'ombe: Mipango thabiti huleta mafanikio katika ufugaji

Mipango thabiti huleta mafanikio katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Wafugaji waliofanikiwa wanafahamu fika kuwa katika uzalishaji wa maziwa 20% inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo.

Tumekutana na kupokea maombi kutoka kwa watu wengi ambao wanataka kuanzisha ufugaji wa ng’ombe, lakini hawajui ni wapi pa kuanzia. Kwa kawaida, wao wanaweka pesa, kutafuta ng’ombe, kununua na mwisho hupata ng’ombe. Hapo ndipo kuhangaika na kupata msongo wa mawazo kwa mfugaji huanza kwa kuwa ng’ombe hazalishi maziwa kutokana na aina yake pekee.

Kwa wafugaji wadogo walio wengi, wakati ambapo ng’ombe anafika zizini kwake wanakuwa bado hawajawa tayari kumpokea ng’ombe huyo kwa ajili ya ufugaji. Ili ujasiria mali kwa njia ya ng’ombe uweze kufanikiwa na kumfaidisha mfugaji kiuchumi, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa miundo mbinu muhimu inakuwa tayari kabla ya kumleta ng’ombe.

Kwa mujibu wa mwongozi wa kitabu cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa Afrika ya mashariki, ng’ombe wa maziwa ni lazima wapate mahitaji yafuatayo:
• Malisho bora na maji safi ya kunywa
• Afya bora bila majeraha
• Mazingira safi ikiwa ni pamoja na  banda lililojengwa vizuri
• Uangalizi mzuri na wa kirafiki,  ambao humfanya ng’ombe kuwa mtulivu bila kuwa na msongo.

Bila mahitaji haya muhimu, na mfugaji kutokumtunza ng’ombe vizuri, asitegemee kuwa ng’ombe huyo atazalisha kiwango kizuri cha maziwa. Uzalishaji wa kiwango cha maziwa na ubora wake unategemeana kwa kiasi kikubwa na mambo hayo yaliyotajwa hapo juu. Wataalamu wanasema kuwa 20% ya uzalishaji wa ng’ombe inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo kutoka kwa mfugaji. Muhudumie ng’ombe wako vizuri naye atarudisha kwa kuzalisha maziwa vizuri.

Mipango

Wafugaji ni lazima wawe na mipango thabiti kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe. Hii hujumuisha idadi ya ng’ombe mfugaji anayotaka kufuga, pamoja na kufahamu ni kiasi gani cha malisho kinachohitajika kwa kipindi chote cha mwaka. Mfugaji pia anapaswa kufahamu kuwa ni kwa namna gani malisho yanafaa kutolewa kwa wanyama.

Mfugaji ni lazima pia apange ni kwa namna gani atapata malisho kwa kipindi chote. Hii inamaanisha kuwa ni muda gani atapanda, kuvuna na kuhifadhi. Mipango ni nguzo muhimu sana kwa kuwa inawezesha kusaidia kufahamu ni nini cha kufanya, namna ya kufikia malengo yaliyokusudiwa, na ni hatua gani imefikiwa. Mfugaji ambaye hana mipango thabiti ni sawa na mtu anayeanza safari bila kufahamu mwisho wa safari yake ni wapi.

Mahitaji ya mlo kamili

Shughuli ya ufugaji wako itakamalika siku ambayo utaweza kuelewa uhusiano kati ya ulishaji wa ng’ombe, uzalishaji wa maziwa na mapato. Endapo ng’ombe wa maziwa atalishwa kwa malisho hafifu ni dhahiri kuwa uzalishaji wa maziwa pia utakuwa hafifu.

Malisho bora

Tafuta ni aina gani ya malisho hufanya vizuri katika ukanda wako. Malisho endelevu hutegemeana kwa kiasi kikubwa na aina ya malisho na utunzaji wake shambani mwako. Chukulia kuwa wewe ni mfugaji mdogo na hauwezi kumudu gharama za umwagiliaji, ni lazima utumie kwa kiasi kikubwa malisho ya wakati wa mvua na kuhifadhi ili kuweza kuyatumia wakati wa kiangazi.

Inashauriwa kupanda majani ya malisho kwa kiasi kikubwa uwezavyo wakati wa mvua. Wahamasishe majirani zako kupanda malisho pia, ili baadaye uweze kununua kutoka kwao. Matete, nyasi, majani ya mtama, majani ya mahindi, lusina, desmodiamu, na alizeti ni miongoni mwa malisho ambayo hufanya vizuri katika maeneo mengi nchini Tanzania.

Kiwango cha kutosha

Fahamu ni kiwango gani kinachotosha kwa kila ng’ombe wako. Hii itakusaidia kufahamu ni kiasi gani cha malisho upande na ni kiasi gani uhifadhi. Kwa wastani, ngombe wa maziwa aliyekomaa mwenye uzito wa kilo 400, anayefugwa ndani ana uwezo wa kula kilo 12 za majani makavu kwa siku. Kumbuka kuwa endapo mifugo yako haitapata malisho ya kutosha wataonesha kwa muonekana wao, na kisha kukupa adhabu kwa kuzalisha maziwa kidogo sana. Kama kanuni inavyoeleza, hakikisha kuwa 15%-18% ya malisho yote ni protini.

Zingatia utunzaji na uzalishaji wa malisho vizuri

Wafugaji walio wengi hukwepa kupanda majani ya malisho kwa kuogopa gharama ya mbolea na mbegu. Kwa uzoefu wetu mfugaji anaweza kutumia mbolea inayotokana na wanyama kupanda malisho na kuyatunza vizuri. Matete ni moja wapo ya malisho hayo. Endapo malisho hayo yatawekwa mbolea vizuri, shamba dogo tu la malisho linaweza kukupatia malisho ya mifugo kwa kipindi chote cha mwaka.

Weka malisho katika hali ya usafi

Hifadhi malisho katika sehemu nzuri, sehemu ambayo hayatapigwa na jua moja kwa moja, mvua au kuwepo uwezekano wa vitu vingine vinavyoweza kuyaharibu kama vile siafu na wadudu wengineo. Majani ya malisho ni lazima yanyaushwe vizuri kuepuka viini vya sumu vinavyoweza kuwepo kwenye malisho. Mfugaji anaweza kuamua juu ya ubora wa malisho kutokana na muonekano wake, harufu na mguso. Malisho mabichi yenye wingi wa majani kuliko shina, yenye kijani kilichokolea, na ambayo yana mguso nyororo, ni moja ya malisho bora ukilinganisha na yale yenye ugumu, shina kubwa na rangi ya njano. Epuka kulisha mifugo yako kwa kutumia malisho yenye ukungu kwa kuwa yanaweza kuwa na sumu.

Kuweka kumbukumbu ni muhimu

Uwekaji wa kumbukumbu ni muhimu lakini huwa hauzingatiwi na wafugaji walio wengi. Baadhi ya wafugaji huona kama uwekaji wa kumbukumbu ni kazi ya ziada, ambayo kulingana na wao haina uhusiano wowote na mapato yanayotokana na shughuli zao. Hata hivyo, bila uwekaji sahihi wa kumbukumbu, mfugaji hawezi kufahamu ni mapato kiasi gani anayopata kutokana na shughuli ya ufugaji. Ni kwa namna gani mfugaji anaweza kufahamu wakati wa kumpandisha ng’ombe wake, kama hajui kuwa zimepita siku ngapi tangu ng’ombe huyo alipozaa!

Kilimo Karanga: Karanga ni zao muhimu la jamii ya kunde

Ni moja ya jamii ya kunde, ambayo hulimwa lengo kubwa likiwa ni uzalishaji wa mafuta, chakula na malisho kwa ajili ya mifugo.

Karanga ni zao maarufu sana duniani katika kilimo cha mzungunguko. Nchini Tanzania uzalishaji wa karanga ni wa chini sana kutokana na kutokuwa na mvua za uhakika, kiwango kidogo cha teknolojia miongoni mwa wakulima, wadudu na magonjwa, pamoja na kutokuwa na mbegu ya uhakika.

Mmea wa karanga ni moja ya mimea mifupi ambayo huota na kuwa na urefu wa sentimita 15-60 kwenda juu. Matunda yake huwa na kati ya mbegu moja mpaka tano, ambapo viriba vyake huwa chini ya ardhi. Mbegu zake huwa na kiasi kikubwa cha mafuta (38% – 50%), protini, kalishamu, potashiamu, fosiforasi, magnesiamu na vitamini. Inasadikiwa kuwa karanga pia zina aina fulani ya viini vinavyotumika kama dawa.

Kiasi kikubwa cha karanga inayozalishwa duniani hutumika kwa kutengenezea mafuta ambayo hutumika kwa kupikia chakula. Makapi yanayotokana na karanga baada ya kukamua karanga ni mazuri sana kwa malisho ya mifugo lakini pia hutumika kwa kutengenezea unga wa karanga ambao kwa kiasi kikubwa hutumika kwa chakula cha binadamu. Karanga pia zinaweza kuliwa zikiwa mbichi, zikiwa zimechemshwa au kukaangwa. Zinaweza pia kutengenezwa kama kitafunwa kwa kuchanganywa na sukari au asali. Pia karanga hutumika kwenye supu, mchuzi, au kama kiungo kwenye aina nyingine za vyakula kama vile nyama na wali. Mabaki ya mimea yake ni malisho mazuri sana kwa wanyama.

Hali ya hewa

Karanga hulimwa kwenye sehemu yenye joto, wastani wa mwinuko wa mita 1500 kutoka usawa wa bahari. Kiwango cha joto kinachohitajika kila siku ni kiasi cha jotoridi 30, na wakati wa ukuaji kinaweza kupungua mpaka jotoridi 15. Hali ya ubaridi huchelewesha karanga kuchanua.

Udongo na kiwango cha maji

Kwa kuwa viriba vya karanga huwa kwenye udongo na ni lazima kuchimbuliwa wakati wa mavuno, huku vikiwa ni vyepesi kuvunjika, ni vizuri kuwa na udongo mkavu, lakini mmea hukua na kustawi vizuri kwenye udongo wa mfinyanzi uliochanganyika na kichanga!

Mvua

Kiasi cha milimita 500-600 cha maji katika msimu wote wa ukuaji wa karanga kinatoa fursa nzuri ya uzalishaji. Hata hivyo karanga ni moja ya mazao yanayostahimili ukame, na linaweza kuvumiliwa ukosefu mkubwa wa maji. Hali inapokuwa hivyo hupunguza kiasi cha mavuno.

Kupanda

Inapendekezwa kupanda kwenye sehemu ambayo udongo una kina na ambao chembechembe zake ni laini.Kuwa makini na uhakikishe kuwa sehemu ya kitalu haina magugu. Kitalu chenye udongo usiokuwa na chembe laini na tambarare inaweza kusababisha upotevu mkubwa wa mimea.

Inapendekezwa kuwa na kiasi cha mimea 200,000 – 250,000 kwenye hekari moja, hasa kwa aina ambayo ni ya muda mfupi. Kwenye nchi nyingi karanga hulimwa kwa kupanda kwenye mistari, ambayo mingi huwa na nafasi ya sentimita 40 x 20 mpaka sentimita 30 x 20.
Baada ya kulima na kusawazisha vizuri, tengeneza matuta yenye mwinuko wa sentimita 80, na sehemu ya juu iwe bapa ili uweze kupanda mistari miwili ya karanga kwenye kila tuta. Ni lazima kuchagua mbegu za kupanda kwa umakini. Ni lazima ziwe safi, zilizojaa vizuri na bila kuwa na mikwaruzo yoyote.

Mbegu zinazokusudiwa kupandwa ni lazima ziachwe kwenye viriba vyake na kumenywa siku chache kabla ya kupanda. Kina cha upandaji wa karanga ni sawa na mahindi ambapo huwa kati ya sentimita 5-8.

Kuna aina mbili za karanga:

• Aina ya mafungu
• Aina inayotawanyika
Aina zinazolimwa Tanzania ni pamoja na Johari, Pendo, Nyota, Sawia, Mamboko.

Kupanda mseto

Karanga hulimwa kama zao linalojitegemea, lakini pia hupandwa mseto na mahindi na hata mihogo. Ni zao zuri pia kuchanganya na mpunga unaolimwa sehemu za mwinuko, mtama, miwa na alizeti. Ili kupata mavuno mazuri inapendekezwa kuwa makini na nafasi tofauti na upandaji wa kienyeji. Kwa maeneo mengine karanga hulimwa kwenye sehemu yenye miti ya mazao ya kudumu kama vile minazi, mipapai, na miti ya mawese. Karanga zinapopandwa mseto na mahindi kwenye sehemu zenye mwinuko husaidia kupunguza mmomonyoko wa ardhi. Mimea ya karanga pia hupunguza uwepo wa vidukari kwa kuwa huwa ni maficho ya wadudu rafiki. Kunakuwa na ongezeko la mavuno ya karanga zinapopandwa mseto na kunde zinazokomaa haraka.

Matunzo

Ili kuwa na mavuno ya hali ya juu, ni lazima magugu yadhibitiwe kabisa. Karanga ni dhaifu sana katika kukabiliana na magugu hasa katika kipindi cha mwanzo cha ukuaji. Ni lazima palizi ifanyike mapema wakati huo miche ikiwa inachomoza kwenye udongo. Miche ikashachomoza palizi ifanyike kwa mikono ili kuepuka usumbufu kwa karanga changa au kuharibu maua. Palizi ya kawaida inaweza kufanyika mpaka kwenye kipindi cha wiki 6 na palizi ya mikono ifanyike baada ya hapo.

Virutubisho pekee vinavyohitajika kwenye shamba la karanga ni kalishamu. Kalishamu hunyonywa moja kwa moja na viriba vya karanga endapo udongo una unyevu unyevu. Kama kutakuwepo upungufu wa kalishamu, viriba vya karanga vitakuwa vitupu bila kuwa na karanga. Mimea inayohitaji Naitrojeni inaweza kupatikana kwa kushirikisha mimea mingine kama vile kunde, badala ya kuweka mbolea ya Naitrojeni kwenye udongo.

Mavuno

Karanga zinazokomaa kwa muda mfupi zinaweza kuvunwa kati ya siku 85-100 tangu kupandwa, na zinazochukua muda mrefu zinaweza kuvunwa katika kipindi cha siku 110-130 tangu kupandwa. Ng’oa mashina machache kuona kama karanga zimeshakomaa. Karanga zilizokomaa ni lazima ziwe na rangi ya kahawia kwa nje, ngumu na zilizokauka.

Kwa kawaida karanga zilizokomaa ndani ya kiriba huwa na rangi ya kahawia, na hutoa sauti inapotikiswa. Magonjwa yanaposhambilia majani ya karanga yanaweza kusababisha karanga kuvunwa kabla hazijakomaa sawa sawa. Ni lazima karanga zichimbwe kwa umakini ili kuepuka karanga kupasuka na kubakia ardhini. Anika kwa siku 2-3, kisha zikwanyue na uanike tena kwenye jamvi kwa siku 7-10 ili kuondoa unyevu kufikia asilimia kumi.

Ubambuaji wa karanga ufanyike kwa mikono au kwa mashine maalum. Karanga zilizopondeka, chafu au kuharibika zitengwe kwani zitapunguza ubora wa karanga na kupunguza bei ya kuuzia. Endapo karanga hazikuhifadhiwa vizuri zinaweza kushika unyevu unyevu ambao husababisha sumu inayojulikana kama aflatoxin ambayo ni hatari sana kwa afya ya binadamu hasa ini. Karanga ambazo zitatumika kwa ajili ya kupanda (mbegu) msimu unaofuata zisibambuliwe kutoka kwenye viriba.

Ufugaji Nyuki: Jenga nyumba ya nyuki upate faida zaidi

Kufuga nyuki na kuzalisha asali kwa mtindo wa kisasa kwa kujenga nyumba ya nyuki inamwezesha mfugaji kuongeza uzalishaji pamoja na kipato.

Chumba cha nyuki 1Ufugaji wa nyuki ni kazi ambayo imekuwepo na kudumu kwa karne nyingi sana. Shughuli ya ufugaji wa nyuki nchini Tanzania hasa katika mkoa wa Tabora ambao ni maarufu kwa uzalishaji wa asali, ilianza kutambulika rasmi tangu mwaka 1884, wakoloni kama vile Rebman na Craft walipofika katika eneo hilo.

Katika kipindi hicho, jamii ya eneo hilo walikuwa wanafuga nyuki kwenye magome ya miti, vibuyu, vyungu, mapango, vichuguu na kwenye miamba. Baada ya muda ufugaji ulipiga hatua kidogo na watu wengi wakawa wanafuga kwa kutumia mizinga iliyochongwa kutoka kwenye magogo ya miti. Ufugaji wa aina hii umedumu kwa karne nyingi kote nchini Tanzania.

Kutokana na uhitaji na ongezeko la matumizi ya bidhaa za nyuki, kulifanyika tafiti mbalimbali ambazo ziliweza kuboresha ufugaji wa nyuki kwa kuwa na mizinga ya kisasa ambayo imewezesha uzalishaji wa asali kuwa mkubwa na kuongeza pato la wafugaji tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Tafiti hazikuishia kwenye kuboresha mizinga tu, ila siku hadi siku kunavumbuliwa namna bora zaidi za kuimarisha uzalishaji wa nyuki. Katika makala hii, tutazungumzia namna ambavyo unaweza kuwajengea nyuki nyumba ili kuboresha mazingira yao ya uzalishaji, na hatimae kupata ufanisi zaidi.

Nyumba ya nyuki

Hii ni aina mpya ya ufugaji wa nyuki ambapo unaweza kujenga kibanda au nyumba kisha kuweka mizinga idadi unayohitaji.

Ni kwa nini kujenga nyumba au kibanda?


• Ni muhimu kufuga nyuki kwenye kibanda au kwenye nyumba kwa sababu inasaidia kudhibiti wizi wa mizinga, pamoja na wanyama wanaokula asali na kudhuru nyuki.
 • Inarahisisha utunzaji wa mizinga na kuwafanya nyuki wasihame kwenda sehemu nyingine.
• Inasaidia watu wengi kujifunza namna nzuri ya ufugaji wa nyuki, ikiwa ni pamoja na watoto, jambo ambalo linafanya shughuli hii kuwa endelevu.
• Ufugaji wa aina hii unasaidia kuwak inga nyuki dhidi ya majanga kama vile moto, na mafuriko.
• Inawaepusha nyuki na usumbufu unaoweza kuwafanya wasizalishe kwa kiwango kinachotakiwa.
• Uzalishaji unaongezeka. Hii ni kwa sababu mizinga inayotumika ni ile ya kibiashara. Mzinga 1 unapata asali kilo 30 sawa na lita 20.


Chumba cha nyukiAina ya nyumba
Unaweza kujenga nyumba yenye upana wa futi 3 na urefu wa futi 9. Nyumba hii inaweza kuchukua mizinga hamsini. Halikadhalika, unaweza kujenga kibanda chenye ukubwa sawa na huo.

Eneo linalofaa

• Ili kuwa na ufanisi mzuri, nyumba hii inafaa kujengwa nje kidogo ya makazi ya watu.
• Kusiwe na mifugo karibu.
•Iwe sehemu ambayo watoto hawawezi kufika.
• Isiwe karibu na njia ambayo watu wanapita mara kwa mara.
• Kusiwe na aina ya mimea ambayo nyuki hawapendi.
• Kuwe na maji karibu.

Mavuno


Baada ya kujenga nyumba, kuweka mizinga na nyuki kuingia, unaweza kuvuna kwa mara ya kwanza baada ya miezi mitatu. Utaweza kupata mavuno mazuri endapo utavuna kabla nyuki na wadudu wengine hawajaanza kula asali.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa wadudu waharibifu kama vile sisimizi, mende na wengineo wanadhibitiwa ili kutokuathiri uzalishaji wa asali. Hakikisha unavuna kitaalamu ili kuepuka upotevu wa asali. Endapo nyuki wametunzwa vizuri na kwenye mazingira mazuri, unaweza kuvuna asali mara tatu kwa mwaka. Katika mzinga mpya nyuki wana uwezo wa kutengeneza masega kwa siku tatu na kuanza uzalishaji wa asali.

Ni nini umuhimu wa asali

• Asali inatumika kama chakula
• Inatumika kama tiba ya magonjwa mbalimbali
• Hutumika kutibu majeraha
• Ni chanzo kizuri cha kipato
• Hutumika katika kutengeneza dawa za binadamu
*Asali inaweza kuhifadhiwa kwa miaka mingi sana bila kuharibika. Hii inatokana na wingi wa dawa maalum iliyo nayo inayofanya isiharibike.


Bidhaa zinazotokana na asali


Chumba cha nyuki 2Kuna aina nyingi ya bidhaa zinatokana na asali, kwa kutengenezwa na nyuki wenyewe na nyingine zikitengenezwa na binadamu kutokana na tafiti mbalimbali. Miongoni mwa bidhaa hizo ni:
• Asali yenyewe
• Royal jelly : Hii ni aina ya maziwa yanayotengenezwa na nyuki, ambayo hutumika kama tiba.
• Gundi: Hii hutumika kutengeneza bidhaa za aina mbalimbali kulingana na mahitaji ya mtumiaji.
• Nta: hutumika kutengenezea mishu maa, kulainisha nyuzi, kutengeneza dawa ya viatu, mafuta ya kupaka, pamoja na dawa ya ngozi.

Kwa maelezo zaidi juu ya ufugji wa kisasa wa nyuki wasiliana na Kinanda Kachelema kutoka SEED Tabora kwa simu +255 783 212 263

Kabichi, faida lukuki kiuchumi na kiafya

Unaweza kulima kabichi msimu wote wa mwaka. Soko lake ni la uhakika katika kipindi chote na ni muhimu kwa afya. Pia, linaweza kutumika kama malisho ya mifugo

Kabichi ni moja ya mazao yaliyomo katika jamii ya mimea inayojumuisha mimea ya kaulifulawa (cauliflower ), kabichi ya kichina na kale. Kwa kawaida kabichi hupandwa kwa msimu mmoja, lakini iwapo itakuzwa kwa ajili ya kutoa mbegu hukuzwa zaidi ya msimu mmoja. Endapo inalimwa sehemu yenye maji ya kutosha, inaweza kulimwa msimu wote wa mwaka. Kichwa cha kabichi kinapofunga vizuri, hutumika kama chakula na huvunwa baada ya kufunga na kukomaa vizuri.

Mizizi: Mizizi ya kabichi hutawanyika ardhini vizuri. Kwa kawaida, huenda chini kiasi cha sentimita ishirini (20 sm), na hujitawanya kwa kiasi cha sentimita sabini na tano (75sm).


Shina: Shina la mmea wa kabichi huwa na rangi ya kijani au zambarau. Hii hutegemeana na aina ya kabichi, na kwa kawaida ni fupi.


Hali ya hewa: Kabichi hustawi vyema katika sehemu yenye hali ya baridi, hali ya joto jingi haifai kwa kabichi kwa kuwa huathiri uotaji na ukuaji wake. Joto jingi pia husababisha kulegea kwa vichwa vilivyofunga. Zao hili hustawi vema katika maeneo yenye mwinuko wa zaidi ya mita 100 toka usawa wa bahari.

Udongo: Zao hili linaweza kustawishwa kwenye udongo wa aina yoyote mradi tu udongo huo usiwe na chumvichumvi nyingi na usiotuhamisha maji. Udongo wa kichanga na ule usio na rutuba ya kutosha husababisha kabichi kukomaa upesi na kuzaa kabichi hafifu zenye vichwa vidogo.

Kitalu: Kitalu ni muhimu katika uzalishji wa zao hili. Ni vema kutengeneza matuta yenye upana wa mita moja, na urefu wowote kulingana na matakwa ya mkulima. Mbolea za samadi na zenye asili ya chokaa zichanganywe vizuri kwenye udongo. Kiasi cha gramu 500 za mbegu huhitajika kwa hekta moja.  Katika upandaji kwenye kitalu ni vizuri kutengeneza mistari katika tuta, umbali toka mstari hadi mstari uwe sentimita ishirini (20). Udongo kiasi kidogo utumike katika kufunika mbegu.

Baada ya mbegu kuota ni vizuri kupunguza baadhi ya miche na uwe katika kipimo cha sentimita 2-3 toka mche hadi mche. Hii itasaidia kuwa na miche mifupi na yenye nguvu. Inafaa kunyeshea kitalu mara moja au mbili kwa siku na katika sehemu za joto ni vizuri kuweka kivuli katika matuta. Katika wiki ya tatu, hadi wiki ya nne, ni vyema kuondoa kivuli kidogo kidogo huku ukipunguza unyeshaji. Hali hii itasaidia miche isipate mshtuko wa uhamishaji shambani.

Kuhamisha na kupanda


Hamisha na kupandikiza miche shambani ikiwa na umri wa wiki nne, wakati huo miche ikiwa na majani manne ya mwanzoni na urefu wa kiasi cha sentimita kumi na mbili (12). Wakati wa upandaji, ni vizuri udongo ukashindiliwa kwenye kila mche. Inafaa upandaji ufanyike mara moja, na ni vizuri ukafanyika nyakati za jioni au asubuhi sana, na udongo uwe na unyevu wakati wote.

Nafasi kati ya mmea

Katika mstari hadi mstari inatakiwa iwe sentimita 60-75. Kutoka mmea hadi mmea ni sentimita 30-60. Pia sentimita 75-90 inaweza kutumika kati ya mstari na mstari.

Mbolea: Ni vizuri kuweka kiasi cha viganja 2-3 vya mbolea ya samadi iliyooza vizuri katika kila shimo.

Palizi: Wakati wa palizi ni vizuri mkulima akawa mwangalifu ili asiharibu mizizi. Wakati kabichi inapoanza kufunga hufunika ardhi, hivyo, husaidia kuzuia magugu yasiote, kwa wakati huu hakuna haja ya kupalilia.


Kuvuna: Kabichi hukomaa katika kipindi cha siku 60-100 tangu kupandwa. Kwa ajili ya kuuza ni vizuri kuvuna wakati vichwa vinapofunga vizuri na huwa na uzito wa kutosha kabichi iangaliwe na kutunzwa baada ya kuvunwa ili isikwaruzwe na kuoza kabla ya kutumiwa. Kwa kawaida hekta moja hutoa mavuno kiasi chatani 50-80.

Aina za kabichi
Kuna aina nyingi za kabichi na zifuatazo ni miongoni mwa aina hizo:
Cabbage Jersey
Early Jersey wakefield – Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5

Cabbage Sugar loaf
Sugar loaf – Aina hii hukomaa mapema sana, kiasi cha miezi 2.5
Cabbage Gloria
Glory of enkhuizen – Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
Prize drumhead Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
Prize drumhead – Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3.5
F1-High Breed Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 2-4
F1-High Breed – Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 2-4
Cabbage Duncan
Duncan – Aina hii hukomaa katika kipindi cha miezi 3


** Majina hayo yanabaki kama yalivyo kutokana na sheria za hati miliki ya watafiti.

Fuga kondoo kisasa uboreshe pato lako

Kwa siku za nyuma, jumla ya idadi ya kondoo wanaofugwa hapa nchini Tanzania ilikaribiana kuwa sawa na idadi ya mbuzi nchini kote. Kwa sasa, idadi ya kondoo imepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na idadi ya mbuzi. Hii imetokana na wafugaji kuhamishia mapenzi yao kwenye ufugaji wa mbuzi.

Kama walivyo mbuzi, kondoo pia wanaweza kufugwa na wafugaji wadogo wadogo na kwenye eneo dogo ambalo hutumika kwa kilimo pia. Kinachotakiwa ni namna ya kuongeza mazao na kuwa na ufanisi. Kwa kuzingatia yafuatayo, mfugaji wa kondoo ataweza kuwa na ufanisi mzuri.
Kondoo hupenda kujilisha kwenye makundi
Kondoo hupenda kujilisha kwenye makundi

Banda la kondoo

Banda na malazi ni lazima yawe mazuri na lenye nafasi ya kupitisha hewa vizuri, linaloweza kuwakinga mifugo dhidi ya mvua, jua na upepo. Sakafu iliyo nyanyuka ni nzuri zaidi.
Lakini sehemu ya mbele ya banda iwe na uwazi. Inashauriwa sakafu iwe na mwinuko kidogo.

Usafi

Ni lazima kinyesi kiondolewe kila siku ili kuweka banda katika hali ya usafi na ukavu kila wakati. Hii, itasaidia kuzuia magonjwa ambayo hushambulia kondoo mara kwa mara kama vile Pneumonia na kuoza kwato, pamoja na kupunguza uwezekano wa kuwepo wadudu nyemelezi.
Kwa kondoo wanaochungwa wakati wa mchana, banda la kawaida lililoezekwa linatosha kuwasitiri kondoo nyakati za usiku. Tenga walau skwea mita 1.5 kwa kila mnyama ili kuzuiuwezekano wa magonjwa yanayotokana na msongamano.

Kwa kondoo wanaolishwa ndani, inatakiwa:

• Sehemu kavu, banda lenye hewa na kuezekwa vizuri (skwea mita 2)
• Kihondi kizuri cha kulishia ili kufanya malisho kuwa safi na kupunguza uharibifu.
• Sehemu nzuri ya nje inayowafaa kondoo kutembea. Tenga walau skwea mita 3 kwa kila kondoo. Kila mwanakondoo anahitaji eneo la kutosha kwa ajili ya kukimbia na kucheza.
• Maji safi na jiwe la chumvi vinahitajika kuwepo wakati wote.
• Utahitajika kuwa na banda la ziada ama kwa muda kwa ajili ya kondoo wenye mimba, kuzalia na kwa ajili ya wanakondoo. Pia, kwa kondoo wanaoumwa.
• Banda la uzio kwa ajili ya kondoo unaweza kuwa rahisi zaidi kwa kuwa kondoo hawaruki wala kupanda juu.

Virutubisho kwa ajili ya kondoo

Kondoo hutumia muda mwingi wakati wa mchana kula majani na baadaye hucheua na kutafuna. Wanapendelea zaidi kula majani na vichaka ambavyo vina mchanganyiko wa madawa ya asili. Wanakondoo hujifunza kutoka kwa mama zao ni nini chakula. Kama unawaanzishia aina mpya ya chakula, lisha kwa kiasi kidogo na uweke kwenye sehemu walikozoea kulishiwa.
Kuwa makini na ukumbuke kuwa wanyama wanaopata lishe duni ni rahisi kushambuliwa na magonjwa na hawana uwezo wa kukabiliana na vimelea vya magonjwa. Kondoo jike asiyelishwa vizuri hawezi kubeba mimba. Uzalishaji wa maziwa pia huwa kidogo kiasi cha kufanya watoto wake kuwa dhaifu na kukua kwa shida.

Kuchunga

Kwa kawaida kondoo wanapenda kulisha kwa kula ardhini, lakini wanakula aina tofauti za majani. Kondoo na ng’ombe wanakuwa na muunganiko na kundi zuri la kujilisha kwa kula majani yaliyomo ardhini. Hii inatokana na kuwa wanyama hawa hushambuliwa na wadudu na magonjwa tofauti na hakuna anayedhuru mwingine. Kondoo hawaogopi mvua kama walivyo mbuzi, lakini kusimama kwenye matope husababisha ugonjwa wa miguu na kuoza kwato.

Ili kuepuka kulisha kupitiliza katika eneo moja, jambo linaloweza kutengeneza na kusababisha vimelea, usiwaache kondoo wako kula sehemu moja kwa muda mrefu zaidi ya wiki 2.

Kila kipande cha uwanda kinatakiwa kuachwa bila kulishiwa kondoo au mbuzi kwa kipindi cha wiki sita. Unahitaji kuwa na walau vipande 4 vya uwanda kwa ajili ya kuchungia kwa mzunguko. Hekari moja yenye malisho mazuri, ni lazima itoe malisho ya kutosha walau kwa kondoo wanne na watoto wao. Gawanya eneo unalohitaji kwa ajili ya kondoo wako mara nne kisha ulishe kwa mzunguko katika eneo hilo.

Kwenye eneo lenye malisho duni unahitaji kuwapatia kondoo eneo kubwa zaidi, na pengine kuwaongezea chakula chenye virutubisho. Tumia majani ya malisho anayozidi wakati wa mvua kutengeneza hay kwa ajili ya kulishia wakati wa kiangazi.